Mshambuliaji wa Kimataifa wa Colombia Radamel Falcao Garcia anatarajiwa kuendelea kubaki England kwenye ligi kuu ya soka nchini humo akiwa na klabu ya Chelsea ambayo siku chache zijazo inatarajia kuthibitisha kumsajili kwa mkataba wa mkopo wa msimu mzima .
Falcao ambaye msimu uliopita aliiwakilisha Manchester United ambako hata hivyo hakuweza kuonyesha cheche zake atajiunga na timu hiyo ya London kwa mkataba wenye thamani ya Euro Milioni 7 huku Chelsea ikiwa na chaguo la kumsajili moja kwa moja endapo itaridhika na kiwango chake.
Wakala wa Falcao, Jorge Mendes amekuwa jijini London kukamilisha masuala kadhaa yaliyozunguka usajili wa mshambuliaji huyo na ndani ya siku chache zijazo anatarajia kuthibitishwa rasmi kama mchezaji wa Chelsea .
Falcao atakuja kuziba pengo la Didier Drogba ambaye ameihama klabu hiyo baada ya kurudi kwa mara ya pili ambapo amecheza kwa msimu mmoja na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya England .
Moja kati ya masuala muhimu yaliyosaidia usajili wa Falcao kwenye klabu ya Chelsea ni ukaribu wa wakala wa mchezaji huyo Jorge Mendez na kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ambapo wakala huyo Mreno pia ni wakala wa The Special One na uwepo wake umekuwa chachu muhimu ya kufanikisha usajili huu .
Usajili huu utacheleweshwa na michuano ya Copa America.. Radamel Falcao atakuwa na jukumu la kuiongoza timu yake ya taifa baada ya kuchaguliwa kuwa nahodha na italazimu kumalizika kwa michuano hii kabla ya kutangazwa rasmi kwa Falcao.