Habari ambazo mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakihofia
kuzipata hivi karibuni hatimaye zimekuwa kweli baada ya kipa namba moja
wa klabu iyo Mhispania David De Gea kuiambia klabu hiyo kuwa anataka
kuhamia Real Madrid .
De Gea kupitia wakala wake ameiarifu United kuwa dhamira yake ni
kujiunga na Madrid na amefikia uamuzi huo baada ya kipindi kirefu cha
kuwaza na kuamua ni hatua ipi bora ya kufuata kwenye mustakabali wake.
De Gea amekaa na United kwa muda wa miaka minne tangu aliposajiliwa
toka Atletico Madrid kwa ada ya uhamisho ambayo iliweka rekodi kwa
makipa ya paundi milioni 17 na amekaa United kwa muda wa miaka minne ,
muda ambao amepia hatua kubwa kiasi cha kufikia kuwa na kiwango cha
ubora wa dunia .
Hivi karibuni De Gea alipewa ofa ya kuongezewa mshahara mpaka kufikia
paundi 200,000 kwa wiki ofa ambayo hajaikubali akiwa amefikia uamuzi wa
kurudi nyumbani kwao kwenye mji aliozaliwa na kukulia huku akipata
fursa ya kuwa karibu na mpenzi wake Edurne.
De Gea amekuwa kwenye mipango ya Real Madrid kwa muda mrefu ambapo
klabu hiyo imemuweka kama chaguo namba moja la kuziba nafasi ya mkongwe
Iker Casillas ambaye umri wake unazidi kuwa mkubwa .
Endapo usajili huu wa David De Gea kuondoka United na kuhamia
Hispania kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu , kipa huyo atakuwa mchezaji
wa tano kuondoka United baada ya Cristiano Ronaldo , David Beckham ,
Ruud Van Nistelrooy na Gabriel Heinze.